WATU wengi wamekuwa wakipenda sana kuandika miswada ya filamu, wakifikiria ama kuwa na matumaini kwamba ni rahisi kwao kuweza kuiuza kwa watayarishaji au makampuni mbali mbali yanayotengeneza filamu nchini, na kujipatia kipato lakini wanasahau kwamba kuna vitu vya msingi sana wamekuwa wakisahau kujiuliza ama kuvitafutia ufumbuzi,
Ukweli ni kwamba ni vigumu sana kuandika mswada “script” na kuuuza hasa katika tasnia inayokua kama ya hapa kwetu Tanzania.
Mara nyingi nimekuwa nikipigiwa simu na watu mbali mbali wakiniambia wao ni waandishi wa miswada ya filamu, na wengi wao tayari wameshaandika miswada kadhaa lakini imekuwa vigumu kwao kupata watu wa kuwauzia ama kununua. Wengine wamefika mbali na kuniambia kwamba wako tayari kuniletea ili niweze kuisoma na kuwatafutia wateja.
Kwa nchi za wenzetu kama Marekani, Ulaya na Asia, uandishi wa miswada ya filamu ni biashara na umekuwa ukiwaingizia vipato vikubwa sana waandishi, watu wengi maisha yao yamekuwa yakitegemea taaluma yao ya uandishi wa miswada kwani katika nchi hizo ni biashara kama biashara nyingine lakini hapa kwetu hicho kitu ni tofauti sana, si ajabu ukaambiwa mtu mmoja ndiye aliyeandika mswada, ameuongoza, na pia ameutayarisha ama kuigiza kama mhusika mkuu.
Kwa mfano gharama ya kuandika mswada mmoja wa filamu katika tasnia za wenzetu kama Hollywood au Bollywood ni kati ya dolla za Marekani 3500 – 50,000 (ambazo ni sawa na shilingi milioni 5 mpaka milioni 70 za Tanzania) kwa mswada mmoja wa filamu, na uandishi wa dibaji gharama yake inaanzia dolla 50 mpaka 500 (yaani shilingi 70,000 – 700,000) kwa dibaji moja. Kwa hapa kwetu imekuwa ni vigumu sana kujua ni gharama kiasi gani watayarishaji wamekuwa wanatumia kununua mswada ama dibaji moja.
Ikumbukwe kuwa ni rahisi sana kuuza “wazo“ kuliko kuuza mswada,lakini wazo pekee haliwezi kumpatia pesa mwandishi kwani mara zote wazo linakuwa ni sentensi moja tu, na wala halina maelezo yoyote ya ziada na yanayojitosheleza, ila ni rahisi sana kuuza wazo likiwa pamoja na dibaji.
Pengine unaweza kujiuliza kuwa dibaji “Synopsis” ni kitu gani hasa katika uandishi wa filamu, kwa maelezo yaliyo rahisi unaweza kuielezea dibaji kama ni maelezo mafupi, ya kina ya namna hadithi itakavyokuwa kwenye filamu unayoiandika, inamwelezea mhusika mkuu jinsi alivyoumbwa, muda ama mahali ambapo tukio lilitokea, dibaji pia inaelezea hasa kile kilichomo ndani ya filamu, Pia inaonyesha mwelekeo wa hadithi bila kuelezea mwisho wake.
Jambo la kukumbuka ni kuwa ili dibaji ikamilike ni sharti ielezee au inabeba dhamira kuu ya mswada wa filamu, lakini filamu nyingine zaweza kuwa na dhamira zaidi ya moja na hapo ndipo changamoto inapoibuka, mswada bora wa filamu ni ule ambao unajengwa na dhamira moja huku dhamira zingine zikifanya kazi ya kuimarisha dhamira kuu.
Ukweli ni kwamba hakuna mtayarishaji au mwongozaji atakayekaa ama kukubali kupoteza muda wake kusoma mswada wa filamu yako wenye kurasa 90, au zaidi na kisha aamue kununua au asiununue, bali itakuwa rahisi kwake kusoma dibaji na kujua kila kitu kilichomo kwenye mswada wa filamu yako. Hivyo inashauriwa kuwa wale wote wanaotaka kuwa waandishi wa miswada ya filamu kuzingatia hatua zote za uandishi ikiwa ni pamoja na kuwa na mawazo mapya, ubunifu wa hali ya juu pamoja na kuzingatia mvuto kwa kile wanachokiandika.
Ili mwandishi yeyote wa filamu aweze kuandika vizuri dibaji nzuri na yenye mvuto ni lazima awe mbunifu na wala asiogope kuandika vitu vingi ama maneno mengi kwani hatua zote za uandishi wa dibaji unaenda sambamba na uhariri wa maneno kuanzia mwanzo mpaka mwisho, lakini kabla haujaanza kuandika dibaji yako yakupasa uzingatie mambo haya; kwanza anza kwa kupanga matukio yote ama vitu vyote vinavyotakiwa kwenye mswada wa filamu “ story lines”, unatakiwa awajue wahusika wakuu wa filamu yako, ni kitu gani kiliwatokea? Je ni matukio gani muhimu yaliyomo katika mswada wa filamu unayoiandika?, je wahusika wakuu katka filamu yako wanatumia mbinu gani kupambana na matatizo wanayokabiliana nayo? Je hadithi yako inaishaje? na je ni mabadiliko gani ya kisaikologia ambayo yanatokea mwisho wa filamu yako?
Jambo la kukumbuka ni kwamba unapoandika dibaji ya mswada wako wa filamu zingatia sana kuwa unaiandika kwa kufuata dhamira kuu inataka nini katika hadithi yako, yakupasa uyajibu maswali yaliyoainishwa hapo juu huku ukiandika kitu ambacho ni cha kipekee na chenye mvuto.
Andika sentensi mbili mpaka tatu ambazo unafikiri zimejibu sawia maswali uliyojiuliza hapo juu, mara zote dibaji safi huwa ni fupi, na inaundwa na sentensi mbili au tatu na mara nyingi haizidi paragrafu moja. Ni ukweli usiopingika kuwa ni kazi ngumu kuandika paragrafu moja ambayo itaibeba filamu nzima ya dakika 90, ni dibaji pekee itakayo mshawishi mtayarishaji ama kampuni kununua mswada wako.
Uandishi wa dibaji ni kitu ambacho hakikwepeki hasa kwa mwandishi bora na makini wa miswada ya filamu, daima nitaendelea kuwasisitizia waandishi wote wa miswada ya filamu wajitahidi kadri ya uwezo wao kuzingatia ubunifu, uadilifu na weledi katika kazi wanazoziandika ili waweze kufikia mafanikio ya waandishi wakubwa duniani waingereza wana msemo unaoseama “easy come easy go” wakiwa na maana kuwa mara zote vitu vitavyokuja kirahisi na vitapotea kwa urahisi pia.
Mwandishi anapaswa kukumbuka kuwa uandishi wa filamu ni kazi kama zilivyo kazi zingine, hivyo asiwe ni mtu wa kujirahisisha, wala kuruhusu chembe yoyote ya dharau kwa kile alichokiandika, ni dhambi kumwachia mtu kazi yako ulioiandika bila makubaliano yoyote ya maandishi, daima mwandishi aliye makini na mwelevu baada ya kuandika dibaji ama mswada kitu kinachofuata ni kusajili wazo na mswada wake katika mamlaka za sheria ilikupata haki miliki ya kazi aliyoiandika, nimekuwa nikisikitishwa na malalamiko ya waandishi wengi wakilalama kuibiwa kazi zao, cha ajabu ni kuwa je mamlaka zinzaohusika na usajili ama haki miliki hazipo au hawazioni? au wanapuuzia halafu wananza kulalamika? Waandishi wa filamu kumbukeni kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala, amkeni na mtetee haki zenu.
No comments:
Post a Comment