My Blog List

Wednesday, December 8, 2010

MWONGOZAJI BORA WA FILAMU ANATAKIWA KUWA NA SIFA GANI?

KATIKA Makala yangu ya wiki mbili zilizopita nilizungumzia ni kwa namna gani mtu anaweza kuwa mwongozaji bora wa filamu, ambapo niliziainisha hatua nne za msingi ambazo wale wote walio na ndoto za kuwa waongozaji bora wa filamu hawana budi kuzifuata ili waweze kufanikiwa.

Ikumbukwe kuwa mwongozaji “ Director” anabeba Majukumu, Mamlaka na anayefanya Maamuzi yote yanayohusu ubunifu katika utengenezaji wa filamu, filamu inapokuwa nzuri na kufanikiwa ni mwongozaji anayepongezwa, na ikitokea filamu haikufanikiwa lawama zote zinamwangukia Mwongozaji.

Kwa kuzingatia uzito na majukumu aliyonayo mwongozaji, ni dhahiri nafasi hii inahitaji mtu mwenye ubunifu na weledi wa hali ya juu,

Je mwongozaji wa filamu anatakiwa kuwa na sifa gani?

Mwongozaji wa filamu anatakiwa awe ni msanii wa kweli, anayejua anachokifanya na anachokitaka , ili mwongozaji aweze kufanya jambo zuri ama kazi nzuri anahitaji kuwa na kipaji, ubunifu, moyo wa kujituma na afanye kazi kwa bidii, huku akitambua kuwa kufanikiwa kwa filamu kunamtegemea yenye kwa kiasi kikubwa, na kwamba kipaji pekee hakitoshi kumfanya mtu aweze kuwa mwongozaji bora.

Ni ukweli usiopingika kwamba huwezi kupima wala kujifunza kipaji, bidii katika kazi, mafunzo, mwelekeo na upeo wa kujua nini unataka kufanikisha ni baadhi ya mambo ya msingi ambayo mwongozaji wa filamu anapaswa kuwa nayo na kuyazingatia.

Sifa kubwa ya mwongozaji wa filamu ni “yule anayeongoza kwa mfano” kila mtu anayehusika katika utengenezaji wa filamu mara zote huwa ana mwangalia mwongozaji , huwa anafanya hivyo kwa lengo la kwenda sambamba na kile anacho kihitaji mwongozaji, kwa sababu mwongozaji ndiye anayebeba roho ya filamu. “Carries a Soul of a Film” Mwongozaji anatakiwa kuwa kiongozi na wakati huo huo afikirie ni kwa namna katika abuni na aingize mawazo mapya kadri inavyowezekana katika filamu anayoiongoza ili iweze kuwa na mvuto. daima afikirie ni kwa jinsi gani utafanikisha utengenezaji wa filamu unayoiongoza na namna utakavyo wasiliana na waigizaji na wafanya kazi anaofanya nao kazi.

Mwongozaji anatakiwa kutambua vipaji , uwezo na madhaifu ya kila mtu anayefanya naye kazi ili aweze kujua ni kwa namna gani atayashughulikia na ni kwa ni kwa namna gani atasafiri nao kimawazo hasa hasa katika kuhakikisha mswada wa filamu unawasilishwa kama ulivyokusudiwa,

Mwongozaji anatakiwa kuwa ni yule mwenye “uwezo wa kufanya maamuzi “ yote yanayohusu utengenezaji wa filamu, kufanikiwa kwa filamu kunamtegemea mwongozaji kwa asilimia 100, ingawa maamuzi yanaweza kuwa mazuri kwa upande mmoja na wakati mwingine yasiwe mazuri, yampasa mwongozaji afanye maamuzi hasa pale anapotakiwa na kuna ulazima wa kufanya hivyo, ila maamuzi yanayofanyika yasiwe ya kumkomoa ama kumuumiza mtu yeyote anayefanya naye kazi bali lengo liwe ni kuboresha na kuongezea radha kwa kile kinachotengenezwa.

Mwongozaji anatakiwa awe mbunifu sana, anatakiwa kujua kila kitu kinachotakiwa katika utengenezaji wa filamu hii ikiwa ni pamoja na kuweza kuwaongoza watu wengi, kujua ni kwa namna gani uigizaji , upigaji wa picha, uhariri, mwanga, mavazi, rangi, maneno , muziki, maeneo n.k vitapangiliwa katika filamu anayoiongoza. Kwa ujumla wake mwongozaji ni lazima ajue kila kitu kinachohusu utengenezaji wa filamu

Mwongozaji anatakiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuwasiliana na wale wote anofanya nao kazi, huku akiwashirikisha kila kitu anachowaza na anachokifikiria lengo likiwa ni kuwafanya wote wasafiri katika mawazo yake ili waweze kutengeneza filamu nzuri.

Waongozaji wengi wanapenda kuwa viongozi “ Leaders” na wanajikuta wanasahau kufanya wanachopaswa, Mwongozaji ni kiongozi wa watu wote anaofanya nao kazi katika utengenezaji wa filamu, utengenezaji wa filamu unahitaji umoja na mshikamano miongoni mwa wafanyakazi na waigizaji, mwongozaji anapaswa kuheshimu mawazo na mchango wa kila mtu, hakuna mtu anayeweza kufanya kazi peke yake “a one man show” hasa katika tasnia ya filamu, ushirikiano ni jambo la muhimu kuzingatiwa .

Kufanya kazi pamoja kuna maana kwamba kuna muunganiko wa mawazo ya watu wengi daima penye wengi hapaharibiki jambo na mawazo ya kila mmoja ni muhimu kuzingatiwa na mchango wa kila mmoja ni muhimu sana katika kutengeneza filamu nzuri.

Ni ukweli usiopingika kwamba hakuna muda wa kutosha kufanya kila kitu unachokitaka na unachokifikiria, Waongozaji wengi wamekuwa wakikata tamaa mapema sana hasa pale kazi inapoonekana kuwa ngumu, mwongozaji anapaswa kutumia vizuri muda alionao kutengeneza filamu nzuri na yenye kuvutia.

No comments:

Post a Comment