My Blog List

Tuesday, January 11, 2011

HUYU NDIYE MWANDISHI BORA WA FILAMU.

Filamu ni njia mojawapo ya kuburudisha na kuielimisha jamii. Utengenezaji wa filamu katika dunia ya leo unawategemea watu wengi sana, lakini jambo la ajabu na ambalo limekuwa likinitatiza siku nyingi ni kwamba, je ni watu wapi hasa muhimu au ili filamu iweze kukamilika inawahitaji watu wangapi? Bila shaka Mtu wa kwanza kukumbukwa ni Mtayarishaji “Producer”, Mwongozaji “Director”, waigizaji “Actors and actresses”.

Ni nadra sana hasa hapa kwetu watu kumkumbuka mwandishi wa mswada“Script writer” hata waandaaji wa tuzo wamekuwa hawawakumbuki kabisa waandishi watu hawa, utasikia tuzo ya Msanii bora wa kike/ Msanii bora wa kiume, Mwongozaji bora, na wala husikii ikizungumziwa tuzo ya Mwandishi bora wa filamu. Je huo ubora wa waigizaji ama ubora wa waongozaji unatoka wapi au na kazi iliyoandikwa na nani?

Ni ukweli usiopingika kwamba Waigizaji, Waongozaji, na hata Watayarishaji wengi wamepata mafanikio makubwa kwasababu walipata mswada mzuri wa kuufuata
Kwa mtazamo wangu nafikiri mwandishi ni mtu muhimu sana hasa linapokuja suala la utengenezaji wa filamu, hata kufanikiwa kwa mwongozaji ama filamu kunamtegemea mwandishi kwa asilimia kubwa, ukweli ni kwamba hata kama mwongozaji atakuwa bora kiasi gani lakini mswada anaoufuata haukuandikwa, wala kupangiliwa vizuri ni dhahiri kunauwezekano mkubwa wa filamu hiyo kuwa mbaya.

Mahitaji ya filamu hapa Tanzania yamekuwa ni makubwa sana hivyo kufanya soko la filamu kukua kila siku, Ukuaji huo umefanya hata mahitaji ya miswada ya filamu kuongezeka pia. Kutokana na mahitaji kuwa makubwa imejitokeza kasumba ya kila mtu kujiita yeye ni mwandishi wa filamu. Je hao wanaojiita waandishi wa script ni Weledi, Wabunifu ama ni wababaishaji tu na wanaandika ili wapate vijisenti vya kuwawezesha waishi mjini?

Waungwana uandishi wa miswada ya filamu ni kazi ngumu sio kama watu wengi wanavyofikiria, ni kazi inayohitaji muda wa kutosha, hivyo ili mtu aweze kuandika mswada bora na utakaouzika hana budi akazingatia sifa za mwandishi bora wa mswada “ a Professional Script Writer”

KIPAJI “Talent ” ni Kitu cha kwanza anachotakiwa mwandishi wa filamu kuwa nacho, lakini ikumbukwe kuwa kipaji pekee hakitoshi kumfanya mtu kuwa mwandishi bora bali kipaji kikubwa na ubunifu, upeo wa kufikiria mambo vitamwezesha kufika mbali, uandishi wa miswada wa filamu unabadilika kila siku kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia na mahitaji tofauti tofauti wa watazamaji wa filamu, kwahiyo ni vizuri mwandishi akajizoesha kwenda sambamba na mabadiliko yanayotokea kila siku, mbinu mojawapo ni kuwa na moyo wa kujifunza ama kusoma au kuhudhuria semina na mafunzo mbalimbali yanayotolewa na wadau au wasomi mbalimbali, pia hata kuhudhuria kwenye matamasha ya filamu, hii itamwezesha kukutana na kubadilishana uzoefu na waandishi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

Uandishi wa filamu sio kwamba unahitaji watu wa aina fulani ama ni kazi ya kundi fulani la watu, la hasha, mtu yoyote anaweza kujifunza na kujiendeleza na kuwa mwandishi bora, kuna shule na vyuo mbali mbali ambavyo vinatoa taaluma ya uandishi wa filamu, hivyo kupitia njia hii mtu anaweza akajiongezea maarifa na ujuzi.
Mwandishi wa filamu ni lazima ajue mahitaji ya jamii anayoiandikia, hili limekuwa tatizo kubwa na sugu kwa waandishi wengi wa miswada ya filamu duniani, wengi wao wamekuwa wanaandika hadithi ambazo haziendani na mazingira halisi ama mahitaji au utamaduni za jamii husika.

Kwa mfano asilimia 75 ya waandishi wa filamu hapa nchini wamekuwa waandika stori ambazo si mahitaji ya jamii ya Tanzania wala hazina maadili wala utamaduni wa kitanzania, wengi wao wanandika hadithi ambazo zinaelezea zaidi maisha ya watu wa ulaya au Afrika ya magaribi.

Ikumbukwe kuwa mwandishi wa filamu ni “ZAO LA JAMII” husika hivyo tunategemea zaidi uandishi wake uzingatie zaidi katika hadithi za maisha ya jamii anayotoka kwa sababu yeye ni mmoja wapo wa wanajamii, hivyo atakuwa anaijua vyema jamii yake bila shaka hata mahitaji ya jamii yake atakuwa anayajua.

Ukiachilia mbali Mwandishi kuwa zao la jamii, mwandishi bora wa filamu ni yule anayejua je ni kundi lipi la jamii amelilenga kuwafikishia ujumbe, ni ukweli usiopingika kuwa kupitia filamu watazamaji wanapata Elimu na burudani pia.
Kwahiyo ujumbe uiopo kwenye filamu ni lazima uende sambamba na mahitaji ya kundi husika.
Mwandishi bora wa filamu anatakiwa kuwa na mawazo mapya, pia akumbuke kuwa uandishi wa miswada ya filamu ni kazi ambayo inawapatia kipato kikubwa waandishi wengi hivyo daima awe ni mtu wa kufikiria kufanya makubwa katika kila kazi anayoiandika, daima alenge kuja na mawazo na mtindo mpya katika kila kazi anayoiandika hii itafanya kazi anazoziandika ziwe na mvuto wa kipekee na hivyo kudumu kwenye jamii kwa muda mrefu.
Daima aweze kusafiri mbali kimawazo zaidi ya vile watazamaji watakavyofikiria, ni dhambi kubwa katika uandishi wa filamu kumpa nafasi mtazamaji wako kuingia ndani ya mawazo katika kazi unayoiandika, andika ukijua kwamba wewe ndio unayemfanya akae na kutizama filamu kuanzia mwanzo mpaka mwisho.

Umakini katika kuchagua vema mtindo wa namna ya kuwasilisha ujumbe ni sifa moja wapo ambayo mwandishi bora wa filamu anatakiwa kuizingatia. Waandishi wengi wanapenda kutumia mtindo wa urejeshi “ flashback’ au mtindo wa moja kwa moja “fore shadowing”, jambo la kuzingatia ni kuwa kila mtindo unafaida na hasara zake, hivyo inampasa mwandishi awe makini sana katika kuchagua ili awasilishe vema ujumbe alioukusudia kwa jamii.

Ukitaka kuwa mwandishi mzuri wa filamu huna budi kuandika mswada utakaowavutia watazamaji na wadau wa tasnia ya filamu, filamu yako ni lazima iweze kuwaburudisha na kuwaelimisha watazamaji kwa huo huo na hasa hasa kuzingatia vile vitu muhimu vinavyotakiwa katika filamu nzuri.

Filamu nzuri ni ile ambayo mwandishi wake ameweza kuyapangilia vizuri matukio na vitendo vingi katika filamu vimeelezea vizuri dhamira ya hadithi nzima, hivyo mwandishi wa filamu anashauriwa aandike vitendo vingi kuliko mazungumzo. Kwani utamu wa filamu ni vitendo na si mazungumzo marefu.

Mwandishi mzuri wa miswada ya filamu ni yule anayeweza kuwashika watazamaji wake kifikra mapema iwezekanavyo, andika mswada ambao utacheza muda wote na fikra za watazamaji wako, daima andika matukio ambayo yatamtamanisha au kumpa hamu mtazamaji na kumfanya asinyanyuke kwenye kiti ama kuzima runinga yake: kwa mfano wahusika wakuu katika filamu yako ni lazima awe anawafurahisha watazamaji wako, kiasi kwamba uwepo wa maadui “Villains” uwafanye pia watazamaji hao hao wanyanyuke kwenye viti hasa pale kunapotokea tukio la kuwakutanisha na kupambana ama kufanya tukio lolote.
Hata Kama unaandika mchezo wa kuigiza, vichekesho, filamu za kutisha, za kisayansi ama za mapenzi kumbuka kwamba siri ya mafanikio ni kuweza kukamata na kusafiri pamoja na fikra za watazamaji wako muda wote.

Uandishi wa miswada ya filamu ni kazi inayotaka mwandishi ajitume sana, awe ni yule mwenye ubunifu wa hali ya juu, upeo mkubwa wa kupambanua mambo, mwenye mawazo mapya katika kila kazi anayoiandika, na anayejua kucheza na saikolojia ya watazamaji wake, kwani uandishi wa filamu unahusisha uwasilishaji wa mtazamo, hisia, matatizo ya jamii inayoandikiwa.

No comments:

Post a Comment